Najda Khan ni Mwanamke ambaye amekua na shauku ya kuishi maisha yake kikamilifu, mbali na kuwa yeye ni mwanamke kama wanawake wengine duniani, amekua na ndoto ya kupata ujauzito kwa muda mrefu bila mafanikio, kwa kipindi cha miaka minane sasa.
''Sijafanikiwa bado lakini sijakata tamaa nitaendelae kujaribu tena na tena'' anasema Bi Khan na kuongeza kuwa:
'' Kwa kweli kama mwanamke saa nyingine unajisikia uko chini sana kutokana na shida hii ya kukosa mtoto , lakini najipa moyo kuwa siku moja nitafaulu" Alisema Najda
Bi Najda mwenye umri wa miaka 34 ni meneja mauzo katika kampuni moja mji mkuu Nairobi Kenya.
Najda yuko katika ndoa ya pili sasa japo hapo awali alikuwa ameolewa lakini ikawa vigumu kwake na mumewe kuendelea kuishi pamoja kutokana sababu nyingi mmojawapo ikiwa ni hali yake ya kutokua na uwezo wa kupata mtoto.
Ndoa yake ya kwanza
Najda Khan alikuwa katika ndoa ya kwanza kwa mwaka mmoja hivi , japo anasema kuwa haikudumu sana lakini muda huo wa ndoa yake haukuwa mwepesi kwake kwani alitamani angelipata ujauzito kwa haraka.
Kwa kawaida ndoa huwa zina changamoto nyingi lakini mojawapo ya changamoto alizozipitia ni tatizo la kutoweza kupata ujauzito, licha ya kujaribu kwa njia ya kawaida ya kupata ujauzito.
"Katika ndoa yangu ya kwanza nilikuwa na imani kuwa ningepata ujauzito, japo tangu usichana wangu nimekuwa na tatizo la maumivu makali wakati wa hedhi, lakini sikudhani kuwa hilo lingekuwa sababu kuu ya mimi kukosa kupata uja uzito " Najda anasema.
Kadri siku zilivyosonga ndivyo Najda na mumewe walivyozidi kutoelewana na hivyo kushindwa kuishi pamoja kama mke na mume na hivyo ikabidi mumewe ampe talaka.
Najda anaeleza kuwa tangu akiwa na umri wa miaka 18, alikuwa na usumbufu wa hedhi zake na alipomtembelea Daktari wa afya ya uzazi katika kliniki, alielezwa kuwa alikuwa na ugonjwa ujulikanao kama Polycystic Ovarian Sydrome, hali hii humsababishia Bi Najda kuwa na matatizo ya homoni na mojawapo ya athari za ugonjwa huo ni kuwa na uzito wa mwili usio wa kawaida na jambo ambalo hadi sasa anapigana nalo sana japo haijawa rahisi.
Alipewa dawa ya kutuliza hali hiyo, Najda amekuwa akipata hedhi zake kila mwezi lakini hajaweza kupata ujauzito.
"Licha ya kuwa mimi sio mlaji wa chakula kingi sana mwili wangu ni mnene kutokana na hitilafu za homoni mwilini, Dakitari hunishauri nipunguze uzito niwe na uwezekano wa kupata ujauzito" Najda aliniambia.
Ndoa ya pili
Baada ya ndoa ya kwanza kuvunjika, Najda hakukata tamaa kwamba ya kumpata mwanaume mwingine ambaye angeelewa hali yake na kumkubali jinsi alivyo.
Miaka minne iliyopita alikutana na mumewe, lakini bado hajajaliwa kupata ujauzito japo anaendelea kuwa na matumaini.
Najda anaeleza kuwa baada ya mumewe kumchumbia, baadhi ya jamaa na marafiki walikuwa tayari wameanza kumweleza mume wake kuwa Najda alikuwa na matatizo ya kizazi na huenda wasifanikiwe kumpata mtoto.
"Baadhi ya watu walijitokeza kabla ya ndoa yangu ya pili , na walianza kumweleza mume wangu kuwa mimi nilikuwa tasa "Najda alieleza.
Najda anasema kuwa alifurahi kwa kuwa penzi kati yake na mumewe lilishinda vita vya maneno kutoka kwa watu ambao wamekuwa wakimkejeli kuwa hana uwezo wa kushika mimba.
Najda ana uzito wa mwili wa kati ya kilogramu 127 na 130 na anasema kuwa Daktari wanasema kuwa uzito huo ni moja ya sababu zinazosababisha yeye kutopata Mimba.
Anasema kuwa kutokana na hayo yeye na mumewe bado wanafikiria iwapo Najda atapitia operesheni za kumsaidia kupunguza uzito au la.
"Kwa kweli uzito wangu wa mwili ni kizuizi kikuu kwangu kupata mimba, lakini nimeshindwa kupunguza uzito na huenda nikahitaji upasuaji", anasema Najda.
Je hali hii ya Polycystic Ovarian Sydrome ni hali gani?
Kulingana na Daktari wa afya ya wanawake Bi Diana Ondieki, hali aliyonayo Najda kwa jina Polycystic ovary syndrome (PCOS) ni hali ambayo kwa kawaida ni hitilafu za homoni za wanawake ambao wamefikia wakati wanapotarajia kuwa wazazi.
Wanawake ambao wana hali hii ya PCOS wanaweza kuwa na hedhi ambazo hazipatikani kwa wakati fulani na wakati mwingine zikija pia zinachukua siku nyingi kabla hazijaisha.
Pia hali hii inaandamana na wanawake kuwa na homoni ambazo zinapatikana miongoni mwa wanaume zikijulikana kama (androgen). Kwa hiyo mayai ya uzazi huenda yakaanza kuota maji na kwa kuwa na hivvyo kumsababishia mwanamke kutokua na uwezo wa kupata mimba.
Jinsi ya kuepukana na ugonjwa wa PCS ni kupitia lishe bora, kufanya mazoezi ya kila mara na pia kupata matibabu yanayofaa kutoka kwa madaktari bingwa wa afya ya uzazi.
0 Comments