Licha ya kwamba hakuna kisa kipya cha virusi vya Corona, lakini serikali ya Kenya imetangaza makatazo mengine kwa umma.
Kuanzia sasa maduka makubwa yameagizwa kudhibiti idadi ya wateja, kipaumbele kikipewa wanawake wajawazito, wazee na walemavu.
Maeneo ya burudani kufungwa ifikapo saa moja unusu usiku kuanzia Jumatatu ijayo kama jitihada za kudhibiti virusi vya Corona.
Awali maeneo ya burudani yaliruhusiwa kuhudumu hadi saa tano usiku.
Daladala zinazobeba watu 14 kwa kawaida sasa zimeagizwa kubeba abiria wanane pekee, yanayobeba watu thelathini kubeba asilimia sitini pekee ya abiria.
Agizo hilo pia linatumika katika usafiri wa treni.
Maafisa wa afya wataanza kunyunyiza dawa za kuua viini katika maeneo ya umma wakianzia soko kubwa la Gikomba, siku ya Jumamosi ambayo pia ni siku ya maombi ya kitaifa.
Waajiri wameagizwa kuhakikisha wafanyakazi wao hawakaribiani na kampuni zitachukuliwa hatua iwapo hawatazingatia hayo na waajiriwa wao watakumbwa na Corona.
Kenya imechukua hatua kadha wa kadha kujaribu kupambana na virusi hivyo ikiwemo kufunga shule na vyuo vikuu kote nchini, kupunguza safari za ndege na kupiga marufuku mikutano ya hadhara na mikusanyiko ya watu.
Aidha Serikali ya Kenya imesema hakuna kisa kipya cha virusi vya Corona katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita na wagonjwa wote saba walioathirika na virusi vya Covid 19 wanaendelea kupata nafuu.
Waziri wa afya nchini Kenya Mutahi Kagwe amesema majuma mawili yajayo yatakuwa muhimu kwa taifa hilo kutathmini juhudi za kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.
Watu kadhaa wamewekwa karantini na wanawafanyia vipimo vya kina kwa watu saba wanaoshukiwa kuambukizwa virusi hivyo.
Maagizo yaliotolewa na wizara ya afya Kenya
1. Kunawa mikono mara kwa mara.
2. Kutokaribiana sana na mtu mwingine ambaye anakohoa ama kupiga chafya - simama umbali wa mita moja
3. Watu wanaokohoa ama kupiga chafya wasalie majumbani mwao ama kutojichanganya na makundi ya watu
4.Hakikisha kwamba unaziba pua na mdomo unapokohoa kwa kutumia kitambaa ama tishu.
5. Mtu anayehisi joto ama tatizo la kupumua ametakiwa kusalia nyumbani.
6. Tumepiga marufuku mikutano ya aina yote ikiwemo ile ya umma kama vile ya kidini, michezo, na wanaotaka kwenda makanisani na msikitini watalazimika kuosha mikono na sabuni kabla ya kuingia katika sehemu hizo.
7. Michezo yote inayohusisha shule imepigwa marufuku lakini shule zote zitasalia wazi kwa wakati huu.
8. Wachukuzi wa umma wametakiwa kuhakikisha kuwa abiria wanaosha mikono yao kabla ya kuingia katika magari hayo.
9. Amewaonya Wakenya kutosambaza habari za uongo kuhusu virusi hivyo katika mitandao ya kijamii ambazo zinaweza kusababisha hofu.
10. Wakenya wamewekewa zuio la kutoka nje ya nchi isipokuwa wale wenye umuhimu mkubwa wa kusafiri na hakuna mtu atakayeruhusiwa kuelekea katika mataifa yenye visa vingi vya ugonjwa huo.
11. Serikali imesema kwamba itatoa maelezo kuhusu ugonjwa huo kila siku.
Waziri huyo amesema kwamba Kenya inaelekea katika wakati ambapo sekta za kibinafsi na zile za kibiashara zitalazimika kuisaidia serikali na raia katika kuchukua jukumu la kukabialana na janga hili.
0 Comments