Vuguvugu limeibuka nchini Tanzania baada ya wafuasi, wadau wa demokrasia na utawala bora kuitika wito wa kukichangia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Mchango huo ni wa kusudio la kupata fedha kulipa faini ya shilingi milioni 350 ambazo wanadaiwa viongozi wa chama hicho kutokana na kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018.
Mbadala wa faini hiyo ni kutumikia kifungo cha miezi mitano jela.
Mjadala mkubwa umetamalaki kutokana na hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba dhidi ya vigogo wa CHADEMA, ambapo hoja
kubwa zimejikita katika uhuru wa Mahakama, vuguvu la wadau wa demokrasia, mshikamano wa wanachama pamoja na viongozi hao kukwepa mtego ambao ungekigharimu chama hicho kwa kupoteza
vigogo kwenye kinyang'anyiro chochote cha kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Mamia ya wafuasi wa CHADEMA na wadau wa demokrasia na utawala bora nchini Tanzania wameitika wito wa kuwachangia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mwenyekiti wa chama hicho na Mbunge
wa jimbo la Hai mkoani Kilimanajro, Freeman Mbowe, Halima Mdee (Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema na mbunge wa Kawe), Esther Matiko (Mbunge wa Tarime Mjini na Mwenyekiti wa chama
hicho kanda ya Serengeti), Esther Bulaya (Mbunge wa Bunda), John Heche (Mbunge wa Tarime Vijijini), John Mnyika (Mbunge wa Kibamba), Peter Msigwa (Mbunge wa Iringa Mjini na Mwenyekiti wa chama
hicho kanda ya Nyasa) na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.
Duru za kisiasa nchini zinaonesha kuwa wimbi la watu wanaokichangia chama hicho ili kuwaokoa viongozi wao, limetafsiriwa kuwa mwanzo wa heka heka za kisiasa, mwamko wa kiu ya demokrasia, uthubutu na uhuru wa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu.
Vigogo hao walitiwa hatiani kutokana na makosa waliyotenda Februari 16 mwaka 2018, katika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni mkoani Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Hati ya mashtaka imeonesha kuwa makosa ya wanasiasa hao ni kula njama, kufanya mikusanyiko na maandamano bila kibali, uvunjifu wa amani pamoja na uchochezi.
Sheria ipi imetumika kuwatoza faini?
Vigogo hao walitiwa hatiani kwa makosa 12 baada ya Hakimu mkazi mkuu kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri.
Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Mwananchi, toloe la Machi 11 mwaka huu lenyewe limeripoti kuwa adhabu ya faini ilisisitizwa mbele ya Hakimu Simba kufuatia maombi ya Wakili mkuu wa serikali, Faraja Nchimbi aliyebainisha kuwa washtakiwa wametenda makosa hayo kwa mara ya kwanza.
Hapo ndipo wakili wa uetetezi, Peter Kibatala alitumia kifungu cha 127 (2) cha sheria ya Kanuni za Adhabu ili walipe faini kama mbadala wa adhabu ya kifungo cha kwenda jela miezi mitano.
Je hukumu hii ina maana gani kwa Chadema?
Dk. Richard Mbunda, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam amemwambia mwandishi, "Kwa mantiki ya muda, hukumu ya viongozi wa CHADEMA imetoka kwa wakati mwafaka kwao, kwani kesi ilikuwa inawapa wakati mgumu. Kwa sababu ni kesi ya jinai, na ingeweza kuathiri ushiriki wao katika uchaguzi endapo hukumu ingekuwa ya kifungo cha zaidi ya miezi sita, lakini sasa wameshajua hukumu kwa hiyo watakuwa huru kushiriki uchaguzi ujao,"
Ameongeza kwa kusema, "Kwa kuzingatia hukumu yenyewe, utagunuda kuwa CHADEMA wamekimbilia kulipa faini bila kujali kiasi cha fedha, kwa kuwa watahitaji kuwa huruma na kutumia vizuri kila dakika kuanzia sasa hadi Oktoba ili kukipa uhai chama chao ambacho hakijashiriki shughuli za siasa kikamilifu kwa muda mrefu."
Je, mshikamano kuwanufaisha kwenye uchaguzi mkuu?
Duru za kisiasa zinaeleza kuwa halikuwa suala la mwenendo wa kesi yenyewe na wahudhuriaji Mahakamani, bali hata matokeo ya hukumu yaliyotolewa yameonesha dhahiri CHADEMA na wadau wa demokrasia wana mshikamano mpya kupitia uchangiaji wa fedha za kulipa faini tajwa na kulitumia suala hilo kuwa mtaji wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu.
Mwitiko wa wafuasi wa CHADEMA na wadau katika harambee ya kuwaokoa viongozi hao na mkono wa dola, zimeonesha kuwa upo uwezekano wa vuguvugu la kimya kimya sawa na kusema mioyo yao imeshikamana kupitia tendo hilo, kuanzia mahakamani ambako mamia ya wafuasi walijitokeza kusikiliza hukumu tajwa hadi kuwanasua viongozi hao kwa kuchangia sehemu ya faini.
Mshikamano huo ni muhimu mno kuelekea uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani. Taswira inayopatikana ni kuanza upya, kukubali mwanzo mpya.
"Lakini naona CHADEMA wanajaribu kutumia hukumu hii kama mtaji, kwa kuibua huruma ya wapigakura. Kwanza wamehimiza kuchangiwa, kitu ambacho kinahamasisha mshikamano wa wanachama na wananchi kwa ujumla. Hamasa hii inaweza kutumika kuwahimiza watu hawa kupigia kura chama hicho ifikapo Oktoba 2020," ameongeza Dk. Mbunda.
Nini tafsiri ya hukumu hiyo kisheria na kisiasa?
Wakili Sweetbert Nkuba, amemwambia mwandishi wa makala haya, "Kisheria imekuwa ya haki na imezingatia hekima ya Mahakama. Kama kifungo kingekuwa kirefu wangepoteza hadhi yao ya ubunge na pengine kukosa sifa za kugombnea katika uchaguzi ujao. Lakini hakimu amezingatia na kutoa kifungo kifupi chenye mbadala wa faini.
"Kisiasa hukumu hii imewainua na pengine wameitumia kama karata ya kuwarudisha kwa wananchi. Chama na wahusika wenyewe wanao uwezo wa kulipa faini lakini hata hivyo wametumia mwanya wa kuwaomba wananchi wawachangie na mwitiko kama ni kweli ama ni wa kutengenezwa kwa vyovyote umewarudisha kwenye mstari sahihi wa kisiasa ukizingatia vyombo vya habari vya nje na ndani vimeliangazia suala lao na kutoa kipaumbele,"
Kwa vyovyote vile CHADEMA na viongozi wake wamepata fursa ya kutengeneza ajenda ya kuingia nayo kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu kupitia kesi zao.
Suala pekee ambalo linasubiriwa kwa sasa ni mazingira ya uchaguzi mkuu iwapo yatakuwa huru,haki na kukidhi viwango vya kimataifa na kuleta athari chanya kwa demokrasia na utawala bora nchini Tanzania.
0 Comments