Coronavirus: Beki wa kati, Daniele Rugani akutwa na virusi , wachezaji wa Arsenal wajiweka karantini

Daniele RuganiHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionDaniele Rugani alishiriki katika mazoezi katika uwanja wa Juventus siku ya Jumanne
Juventus imetangaza kwamba beki wa kati wa Italia Daniele Rugani amekutwa na virusi vya corona.
Klabu hiyo ya ligi ya Serie A imesema kwamba imechukua hatua zote za kumtenga mchezaji huyo zinazohitajika kisheria ikiwemo kuwashirikisha wale ambao waligusana naye
Klabu hiyo imeongezea kwamba Rugani mwenye umri wa miaka 25 kufikia sasa hajaonesha dalili za ugonjwa huo.
Michezo yote nchini Italia imeahirishwa hadi Aprili 3 huku taifa hilo likijiweka katika karantini kutokana na mlipuko huo wa coronavirus.
Rugani ameichezea klabu yake mara saba pekee msimu huu na hakutumika katika mechi ya Juventus dhidi ya Intermilan ambayo klabu hiyo iliibuka na ushindi wa 2-0 katika mechi iliochezwa bila mashabiki siku ya Jumapili.
Mechi ya Inter iliotarajiwa kucheza dhidi ya Getafe katika michuano ya Europa siku ya Alhamisi pia imeahirishwa.
Rugani ameshinda mataji manne ya ligi ya Italia akiichezea Juventus na aliichezea Italia mara saba, mara ya mwisho ikiwa 2018.
Siku ya Jumapili alichapisha picha mtandaoni katika chumba cha maandalizi cha Juve akisherehekea ushindi wa klabu hiyo dhidi ya Inter pamoja na wachezaji wenzake.
Italia imerekodi visa 12,000 vya maambukizi na vifo 827 kutokana na virusi hivyo.
Wakati huohuo mechi kati ya Arsenal na Manchester City imeahirishwa baada ya kuwepo kwa hofu ya virusi vya corona, huku baadhi ya wachezaji wa Arsenal wakiamua kujitenga baada ya mmiliki wa klabu ya Olympiakos Evangelos Marinakis kupatikana na virusi hivyo.
Arsenal inasema kwamba Marinkis mwenye umri wa miaka 52 alikutana na baadhi ya wachezaji wake wakati Arsenal walipokuwa wenyeji wa mechi na klabu hiyo katika kombe la Europa wiki mbili zilizopita.
MarinakisHaki miliki ya pichaREX FEATURES
Image captionMmiliki wa klabu ya Olympiakos Marinakis
Marinakis ambaye pia anaimiliki klabu ya ligi ya daraja la kwanza nchini England Nottingham Forest alisema siku ya Jumanne kwamba amepatikana na virusi vya corona.
Arsenal inasema kwamba baadhi ya wachezaji wake walikutana na mmiliki wa klabu hiyo ya Olympiakos.
''Ushauri wa kimatibabu tuliopatiwa ni kwamba tayari wachezaji hao wapo katika hatari ya kupatikana na virusi hivyo , hivyo basi tumewataka kujitenga kwa muda wa siku 14 kutoka siku waliogusana na Marinakis.
Ni kutokana na hilo kwamba wachezaji hao hawatashiriki mechi iliopangwa kuchezwa dhidi ya Man City na ligi ya England imeamua kwamba mechi hiyo iahirishwe kwa mara ya pili. Wachezaji hao watajitenga kwa siku 14 ''.
Wafanyakazi wanne wa Arsenal ambao walikuwa wameketi karibu na Marinakis wakati wa mechi hiyo pia watasalia nyumbani hadi siku 14 zitakapokamilika.

Post a Comment

0 Comments