
Wizara ya afya nchini Kenya imethibitisha kisa kingine kimoja cha maambukizi ya virusi vya corona.
Mtu huyo hahusishwi na mtu wa kwanza aliyethibitika kuwa na maambukizi.
Mtu huyo alisafiri kutoka Uingereza tarehe 8 mwezi Machi 2020 na kuwasili Kenya tarehe 9 mwezi Machi mwaka huu.
Katika hatua nyingine, kanisa la kianglikani nchini humo limesitisha ibada zote kuanzia leo Machi, 17 mwaka 2020.
Kasisi Dkt. Jackson Ole Sapit ametoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa wakati huu wa kwaresima, ambao ni wakati wa kufunga na kusali watu wanapaswa kusali wakiwa nyumbani na si kwenda kanisani ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.Kutokana na huduma hizo za ibada kusitishwa kwa muda wa siku 30 basi kanisa litaweza kutoa huduma za kiroho kwa njia mbadala kwa kushauri wakristo kusali wakiwa nyumbani ili kuzuia mikusanyiko ya watu wengi.
Huduma kama ibada za jumapili, mazishi na harusi zitazuiwa kuwa na mkusanyiko mkubwa
Ingawa wakristo wanakumbusha kuiombea nchi hiyo jumapili, Machi, 22.

Hapo jana, Msemaji wa serikali ya Kenya Kanali mstaafu Cyrus Oguna amesema watu wengine watatu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona wameripotiwa.
Watu wengine 14 bado wako karantini wakisubiri majibu.
Akizungumza jioni hii, Oguna ameongeza kuwa watu wote hao ni kutoka nje ya nchi hiyo na hatua zinachukuliwa kuhakikisha kuwa hakuna ripoti mpya za maambukizi.
Kanali Oguna amesema serikali inahakikisha kuwa idadi ya watu walioambukizwa haizidi iliyopo hivi sasa.Gazeti la The standard limeripoti
Kisa cha kwanza cha virusi vya corona Kilithibitishwa nchini Kenya. Waziri wa afya nchini humo Mutahi Kagwe alithibitisha kisa hicho katika tangazo alilolitoa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari.
Nchini Ethiopia mamlaka za nchi hiyo pia imetangaza kisa cha kwanza cha maambukizi ya coronavirus. Mgonjwa wa Ethipia ni raia wa Japan.
Bwana Mutahi amesema kwamba mtu mwenye maambikizi ya virusi vya Corona alithibitishwa kuwa ana maambukizi hayo Alhamisi usiku.
Waziri huyo amesema kwamba kisa hicho ni cha kwanza kuripotiwa nchini Kenya tangu kuzuka kwa mlipuko huo mjini Wuhan nchini China.

Nini kilichotokea
Kisa hicho ni cha raia wa Kenya aliyewasili nchini humo kutoka Marekani kupitia mjini London nchini Uingereza tarehe 5 mwezi Machi 2020.
Aligunduliwa kuwa na virusi hivyo katika maabara ya wizara ya afya nchini Kenya.
Hatahivyo waziri huyo amesema kwamba mgonjwa huyo ambaye ni mwanamke yuko katika hali njema na kwamba viwango vyake vya joto vimeshuka na kuwa vya kawaida.

''Tarahe 5 mwezi Machi aligunduliwa kuwa na virusi hivyo katika maabara ya serikali lakini sasa viwango vyake vya joto vimeshuka na kuwa vya kawaida anakula vizuri lakini hawezi kutolewa hadi virusi hivyo vitakapokwisha mwilini.'', amesema Waziri Kagwe.
Wakenya wametakiwa kutokua na hofu
Waziri huyo amewataka Wakenya kuwa watulivu na kuacha wasiwasi.
Amesema kwamba serikali ya Kenya kupitia wizara ya afya itaendelea kuimarisha mikakati ili kuhakikisha kwamba hakuna usambazaji wa virusi hivyo zaidi.
- Majibu ya maswali kumi yanayoulizwa sana kuhusu coronavirus
- Kocha wa Arsenal na mchezaji wa Chelsea wakutwa na virusi vya corona
Kamati ya dharura ilioanzishwa ili kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona itaendelea kutoa muongozo ili kukabiliana na ugonjwa huo hatari.
Amewahakikishia Wakenya kwamba Kenya imejiandaa vilivyo kukabiliana na virusi hivyo tangu kisa cha kwanza kitangazwe nchini China, akiongezea kuwa serikali itatumia raslimali zake zote kukabiliana na janga hili..

Amesema kwamba tayari serikali imetambua maeneo yote ambayo muathiriwa alipitia kabla ya kufanyiwa vipimo.
''Mtu anapoambukizwa huhisi maumivu machache na kupona kwa urahisi lakini virusi hivyo vinaweza kuwaathiri zaidi watu wengine hususan wazee na wengine wenye magonjwa sugu''.

Kutokana na hatua hiyo serikali imevunja sheria ya maeneo ya umma na kuwataka Wakenya kufuata maagizo yafuatayo.
Maagizo yaliotolewa na wizara ya afya Kenya
1. Kunawa mikono mara kwa mara.
2. Kutokaribiana sana na mtu mwingine ambaye anakohoa ama kupiga chafya - simama umbali wa mita moja
3. Watu wanaokohoa ama kupiga chafya wasalie majumbani mwao ama kutojichanganya na makundi ya watu
4.Hakikisha kwamba unaziba pua na mdomo unapokohoa kwa kutumia kitambaa ama tishu.
5. Mtu anayehisi joto ama tatizo la kupumua ametakiwa kusalia nyumbani.
6. Tumepiga marufuku mikutano ya aina yote ikiwemo ile ya umma kama vile ya kidini, michezo, na wanaotaka kwenda makanisani na msikitini watalazimika kuosha mikono na sabuni kabla ya kuingia katika sehemu hizo.
7. Michezo yote inayohusisha shule imepigwa marufuku lakini shule zote zitasalia wazi kwa wakati huu.
8. Wachukuzi wa umma wametakiwa kuhakikisha kuwa abiria wanaosha mikono yao kabla ya kuingia katika magari hayo.
9. Amewaonya Wakenya kutosambaza habari za uongo kuhusu virusi hivyo katika mitandao ya kijamii ambazo zinaweza kusababisha hofu.
10. Wakenya wamewekewa zuio la kutoka nje ya nchi isipokuwa wale wenye umuhimu mkubwa wa kusafiri na hakuna mtu atakayeruhusiwa kuelekea katika mataifa yenye visa vingi vya ugonjwa huo.
11. Serikali imesema kwamba itatoa maelezo kuhusu ugonjwa huo kila siku.
Waziri huyo amesema kwamba Kenya inaelekea katika wakati ambapo sekta za kibinafsi na zile za kibiashara zitalazimika kuisaidia serikali na raia katika kuchukua jukumu la kukabialana na janga hili
0 Comments